FAO in Tanzania

Taarifa sahihi za viwango na aina ya samaki tulionao kuchochea ujenzi wa viwanda vya kusindika samaki nchini

Wageni waalikwa katika hafla hiyo
19/04/2018

Meli ya kisasa ya utafiti wa samaki na mazingira bahari ya Dkt. Fridtjof Nansen imekamilisha uchunguzi wake wa rasilimali na mazingira bahari katika maji ya Bahari ya Hindi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hii ni meli ya tatu kubeba jina hili katika miaka 40 ya ushirikiano wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na nchi ya Norway. Ikiwa na maabara saba tofauti zenye vifaa vya kisasa kabisa, meli hii ya Dkt. Fridtjof Nansen ni chombo pekee cha majini chenye kupeperusha bendera ya Umoja wa Mataifa.  Chombo hiki kinaendesha tafiti kwenye nchi mbali mbali lengo likiwa kukusanya taarifa kuhusu mtawanyiko na uwingi wa samaki, bionuwai, hali za mazingira, na shughuli nyingine nyingi kwa kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa kabisa kusaidia nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania kukusanya taarifa za kisayansi muhimu kwa ajili ya uvuvi endelevu na kujua namna mabadiliko ya tabia nchi yanavyoathiri bahari zao. 

Chini ya Mpango wa Programu ya EAF-Nansen inayofadhiliwa na Norway na kutekelezwa na FAO kwa kushirkiana na Taasisi ya Utafiti wa Mambo ya Bahari ya Norway (IMR) meli hii inaendesha utafiti wake wa rasilimali bahari na mazingira baharini katika ukanda wa Kusini Mashariki mwa Afrika na Bahari ya Hindi. Chini ya Programu hii, nchi thelathini (30) za Kiafrika ikiwemo Tanzania zitapata msaada wa kitaalam na kisayansi wa namna ya udhibiti wa rasilimali zao za samaki na viumbe bahari wengine kutumia na kutekeleza mpango endelevu wa utunzaji wa mazingira.

Akizungumza siku ya Alhamisi katika hafla fupi ya kilele cha utafiti huo katika pwani ya Tanzania iliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam ndani ya meli ya Dkt. Fridtjof Nansen, Katibu Mkuu Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Mhandisi John William Kijazi alisema utafiti huo umekuja kwa wakati muafaka kwani ilikuwa inaenda kuongeza kasi ya uanzishwaji wa viwanda hapa nchini hususan katika sekta ya uvuvi. Alikuwa anamwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli katika hafla hiyo.

“Hii ni hatua kubwa sana kwa Tanzania ambayo itafaidika na huduma za utafiti wa kisasa wa meli hii kupitia ushirikiano wa wadau hapa nikizungumzia FAO na Serikali ya Norway, kuweza kujua kwa uhakika aina na kiwango cha samaki na rasilimali bahari nyingine tulizonazo katika maji yetu,” alisema na kuongeza: “Taarifa kuhusu rasilimali bahari zetu zitakuwa muhimi sana katika kufanya maamuzi na kupata fursa za ndani na kimataifa za uwekezaji katika sekta ya uvuvi huku tukitilia maanani mambo muhimu ya utunzaji wa mazingira. Kwa kutumia taarifa sahihi tunaweza kuwavutia wawekezaji waje na kujenga viwanda vya kusindika samaki na vingine vinavyohusiana na sekta hii ya uvuvi na hivyo kuongeza kasi kwenye mpango wetu wa kujenga Tanzania ya viwanda.”

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh.Luhaga Joelson Mpina, alisema kuwa ni matumaini ya Serikali kwamba takwimu zitakazotokana na utafiti huo zitaisaidia Tanzania kujua kwa uhakika juu ya aina na kiwango cha samaki na rasilimali bahari nyingine katika eneo letu la Bahari ya Hindi. “Hii itatuwezesha kupata wawekezaji katika eneo hili ambao watajenga viwanda vya kuchakata na kusindika mazao ya samaki ambapo mbali ya kutoa fursa za ajira kwa watu wetu hususan vijana katika mnyororo wa thamani, lakini pia utakuza mapato ya serikali,” alisema.  

Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania, Fred Kafeero, alisema kuwa ushirikiano na Serikali ya Norway katika kutekeleza Programu ya Nansen ni wa umuhimu wa kipekee kwa FAO. “Mbali ya taarifa ambazo zitawezesha udhibiti bora wa rasilimali kwa matumizi endelevu, utafiti huu utapekelea uelewa mzuri wa athari za mabadiliko ya tabia nchi na athari nyingine za nje, kama vile uchafuzi wa mazingira na mifumo ya uhai baharini.,” alisema.

Kwa upande wake, Balozi wa Norway hapa nchini Bi. Hanne-Marie Kaarstad, alisema: “Ni matumaini yetu kuwa meli ya Nansen itachangia sio tu katika kuhakikisha kuwa takwimu za uhakiki za kisayansi zinapatikana, lakini pia kuimarisha uwezo katika matumizi ya takwimu hizo ili kujenga mikakati bora ya udhibiti na matumizi ya rasilimali bahari. Bahari zina utajiri mkubwa kuanzia ufugaji wa samaki, uvuvi na pia uchakataji na usindikaji wa mazao ya samaki. Sera zenye kutilia maanani taarifa hizi ni muhimu katika kujenga msingi kwa ajili ya viwanda vipya kama vile uchimbaji wa madini katika sakafu ya bahari na kilimo pamoja na uvunaji wa mwani na viumbe vingine, na hivyo kuchangia katika juhudi za maendeleo kwa Tanzania.”

Hafla hii iliandaliwa kwa pamoja kati ya FAO kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway hapa nchini na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na ilihudhuriwa na Mawaziri kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, Mabalozi na wakuu wa Mashirika na Taasisi za Kimataifa na Umoja wa Mataifa nchini Tanzania.

Chimbuko

Programu ya Udhibiti na Matumizi Endelevu wa Rasilimali Samaki (EAF) – imekuwa ni moja ya marejeo makuu za FAO katika kusaidia nchi katika juhudi zao za kudhibiti na kutekeleza kanuni za maendeleo endelevu. Kanuni za FAO za Uvuvi Sahihi na pia sheria nyingi za kimataifa zinaangazia faida ambazo zinaweza kupaikana kupitia programu wa EAF. EAF ni njia ya kutekeleza nyingi ya Kanuni Sahihi za Uvuvi kwa kutoa muongozo wa namna ya kufikia malengo sera ya kiuchumi, kijamii na ikolojia kupitia malengo, viashiria na njia za tathimini. EAF inanuia kuweka uwiano kati ya mambo mawili muhimi: utunzaji wa mazingira na mifumo ya ikolojia kwa upande mmoja  na kuweza kutatua mahitaji ya binadamu ya chakula na faida za kiuchumi upande mwingine.

Serikali ya Tanzania kutipitia Wizira ya Mifugo na Uvuvi na FAO wamesaini mkataba wa programu ya ushirikiano kwa ajili ya utekelezaji wa Programu ya EAF-Nansen huku Taasisi ya Utafiti wa Mambo ya Bahari ya Norway (IMR) ikitoa huduma ya za kisayansi. Programu mpya ya EAF-Nansen imeongeza eneo jipya la kushughulikia ambalo linaangalia athari za tofauti na mabadiliko ya tabia na uchafuzi wa mazingira yanavyoathiri uzalishaji wa mazingira bahari na afya.