FAO in Tanzania

FAO yasaidia nchi za Afrika kuandaa taarifa kuhusu rasilimali zao za misitu

Dkt. Mushumbusi akiongea wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo
20/09/2018

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) linaendesha warsha ya wataalam wa misitu kutoka katika nchi za Afrika zinazozungumza Kiingereza jijini Dar es Salaam ambapo wanategemewa kupeana uzoefu na kutoa taarifa za maendeleo ya uandaaji wa ripoti za Tathmini ya Rasilimali za Misitu ya Dunia kwa mwaka 2020.

Akizungumza katika ufunguzi wa warsha hiyo ya kikanda, Kiongozi wa Timu ya FAO inayeshughulikia Tathmini ya Rasilimali za Misitu ya Dunia, Anssi Pekkarinen, alisema mkutano huo unalenga kuangalia ripoti ya nchi husika za tathmini ya rasilimali misitu kwa ajili ya mwaka 2020 na kwamba lengo ni kuchangia katika kuboresa, usahihi, ukamilifu na uwazi wa ripoti husika na takwimu zilizotumika.

Fursa muhimu

“Warsha hii itatoa fursa kwa wataalam wa misitu wa nchi husika, wanaoshughulikia suala la Tathmini ya Rasilimali za Misitu ya Dunia, kuwasilisha taarifa za maendeleo ya uandaaji wa ripoti za nchi zao, kuzipitia pamoja  na wataalam kutoka FAO and kushirikiana uzoefu na changamoto pamoja na washiriki kutoka nchi nyingine ili kupata ufumbuzi,” alisema.

Kwa mujibu wake, FAO imekuwa ikifanya tathmini hizi za rasilimali misitu za dunia toka mwaka 1948 na kwamba mwaka huu ilikuwa inasherehekea kumbukumbu ya miaka 70 ya zoezi hilo ambalo limekuwa likibadilika kila mara ili kutilia maanani mabadiliko katika mahitaji ya taarifa.

Muhimu kwa Tanzania na nchi nyingine

Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania, Dkt. Revocatus Petro Mushumbusi, alisema warsha hiyo imekuja wakati muafaka na kwamba ni ya umuhimu mkubwa kwa Tanzania nan chi nyingine zote zinazohusika.

“Ni matumaini yetu kuwa majadiliano kwenye mkutano huu yatatoa fursa ya kipekee na sahihi ya kusaidia zoezi la tathmini na ufuatiliaji wa a rasilimali misitu katika nchi zetu kwa ajili ya kufanya maamuzi sahihi,” alisema.

Dkt. Mushumbusi alikuwa anazungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kitengo cha Misitu na Ufugaji Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii.

Uimarishaji wa Uwezo

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mwakilishi wa Shirika la FAO katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Fred Kafeero, alisema kuwa Shirika hilo la Umoja wa Mataifa linatambua umuhimu na mchango wa wataalam wa misitu wa nchi husika wanaoshughulikia suala la Tathmini ya Rasilimali za Misitu ya Dunia katika mchakato huo.

“Mkutano huu utatoa fursa ya kupitia rasimu za ripoti za nchi husika na kufaidika na uzoefu kutoka kwa washiriki kutoka nchi mbali mbali kwenye ukanda huu pamoja na FAO ambao ni wataalam kwenye masuala haya. Hii ni moja ya njia nyingi ambazo FAO inatumia kuimarisha uwezo wa nchi wanachama,” alibainisha.