FAO in Tanzania

FAO yaikabidhi Serikali rasimu ya Sera ya Taifa ya Misitu baada ya mapitio

Mej. Jen. Milanzi akionesha nakala za rasimu baada ya kuzipokea kutoka kwa Mwakilishi wa FAO, Fred Kafeero, (wa pili kutoka kulia). Kushoto ni Mkurugenzi wa Misitu, Dkt. Ezekiel Mwakalukwa.
10/04/2018

LEO, Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limekabidhi rasimu ya mwisho ya Sera ya Taifa ya Misitu kwa Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii (WMU) kufuatia kukamilika kwa mchakato uliowashirikisha wadau wote muhimu.

Mwezi Februari mwaka 2017, FAO na Serikali ya Tanzania kupitia WMU zilisaini mkataba wa msaada wa kitaalam kuisaidia Serikali kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Misitu ambayo ilipitishwa mwaka 1998.

Chini ya mkataba huo, FAO ilikuwa inaenda kutoa msaada wa kitaalam wenye thamani ya Shilingi za Kitanzania milioni 280/- kwa Tanzania kuwezesha kukamilishwa kwa mchakato wa mapitio wa sera hii.

Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika katika makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii mjini Dodoma baina ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, na Mwakilishi Mkazi wa FAO hapa Tanzania, Fred Kafeero.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Mej. Jen. Milanzi kwa aliishukuru FAO kwa msaada wake akisema kuwa ulikuja kwa wakati muafaka wakati ambapo nchi ilikuwa inahitaji sera dhabiti kukabiliana na masuala mbali mbali yanayohusu sekta ya misitu. “Nchi inakabiliana na changamoto kadhaa katika kudhibiti rasilimali misitu na ndio maana tulianzisha mchakato wa kuipitia sera yetu ya misitu kwani iliyopo sasa ni ya zamani sana ikishindwa kuendana na kuakisi maendeleo mengi ya sasa, yakiwemo malengo ya maendeleo endelevu,” alisema.

Mafanikio makubwa

Kwa upande wake, Bw. Kafeero alisema kuwa FAO inayo furaha kubwa kuona kiwango cha mafanikio kilichofikiwa katika mchakato huo. “Tayari FAO imesaidia nchi nyingi kwenye maeneo kama haya. Msaada unahusisha uwezeshaji wa ushiriki wa washikadau kutoka sekta mbali mbali ukijumuisha wadau wa kitaifa na kimataifa. Lengo ni kuhakikisha kwamba sera hii sio tu inatilia maanani mambo ya hapa nyumbani, lakini pia mahitaji ya masuala ya maendeleo ulimwenguni,” alisema.

Kwa mujibu wake, mchakato huu wa mwaka mzima ulikuwa shirikishi na ambao uliwaleta pamoja washikadau muhimu kushirikiana mawazao na michango mbali mbali iliyojumuishwa kwenye sera hii ya misitu. Kwa nyongeza, ilikuwa ni fursa ya kuangalia masuala makuu yanayoathiri sekta ya misitu katika ngazi ya kitaifa na kimataifa, ikijumuisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, na Mkataba wa Mabadiliko ya Tabia Nchi wa Paris. Bw. Kafeero alisema misitu ni moja ya maeneo ya majukumu makuu ya FAO kwa kuwa ni moja ya maeneo muhimu yanayohusiana na matumizi endelevu ya maliasili, uhakika wa chakula na lishe pamoja na maendeleo ya uchumi kwa ujumla.

Hatua zinazofuata

Wakati huo huo, FAO pamoja na Serikali wanamalizia taratibu za kuandaa mkakati wa kuitekeleza hii Sera ya Kitaifa ya Misitu.